China ikiwa ni nchi mshiriki maalum wa maonesho ya 61 ya kimataifa ya vitabu ya Frankfurt, tarehe 14 iliitisha mkutano wa ngazi ya juu ya uchapishaji wa kimataifa huko Frankfurt. Wajumbe wa wachapishaji maarufu kutoka nchi mbalimbali walichambua changamoto mbalimbali zinazozikabili shughuli za uchapishaji za hivi sasa, pia walibadilishana maoni na hatua za kuzikabili na changamoto. 
Katika miaka ya hivi karibuni, shughuli za uchapishaji zinakabiliwa na changamoto kutoka sekta mbalimbali zikiwemo teknolojia, soko, mitaji na kusoma. Hasa baada ya msukosuko wa fedha duniani kutokea mwaka 2008, shughuli za uchapishaji za nchi mbalimbali zote zimeathiriwa. Lakini kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa shirika kuu la habari na uchapishaji la China Bw. Liu Binjie alisema shughuli za uchapishaji nchini China inaendelea kupata maendeleo mapya. Kulingana na hali mbaya ya idara zingine za fedha, ukubwa wa shughuli za uchapishaji umeongezeka zaidi.
Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2008 China ilichapisha aina za vitabu laki 2.75, kwa jumla ilichapisha vitabu bilioni 7. Ikilinganishwa na kiwango cha mwaka jana, aina za vitabu zimeongeza asilimia 11.03, na idadi ya vitabu kwa jumla imeongeza asilimia 10.21. China ikiwa ni nchi kubwa ya uchapishaji, inaendelea kudumisha ongezeko la kasi katika upande wa uzalishaji na mauzo ya vitabu na matumizi ya karatasi.
Katika miaka ya hivi karibuni, siyo shughuli za jadi za uchapishaji tu, bali pia shughuli za uchapishaji wa kitarakimu zimepata maendeleo ya kasi. Shughuli mpya za uchapishaji ambazo alama yake ni kuchapisha vitabu vya kitarakimu sasa zimekuwa sehemu muhimu kwa ukuaji wa shughuli za uchapishaji. Kulingana na takwimu, kufikia mwishoni mwa mwaka 2008, katika makampuni 578 ya uchapishaji nchini China, asilimia 90 kati yao, yameanzisha huduma za kuchapisha vitabu vya kitarakimu. Vitabu vya kitarakimu vimechapishwa zaidi ya milioni 30, na mapato yamefikia yuan milioni 300, kiasi hiki kimeongeza asilimia 50 kuliko kiwango cha mwaka 2007. Bw. Liu alidokeza kuwa, mwaka 2009 mapato ya uchapishaji wa vitabu vya kitarakimu yatazidi mapato ya uchapishaji wa vitabu vya karatasi kwa mara ya kwanza.
Ingawa shughuli za uchapishaji nchini China zimepata maendeleo ya kasi katika miaka ya hivi karibuni, lakini haiwezi kupuuza athari inayoletewa na msukosuko wa fedha duniani. Sekta za vitabu, magazeti na shughuli za uchapaji zote zimeathiriwa na msukosuko huo. Lakini naibu mkurugenzi mtendaji wa shirika la uchapishaji la China Bw. Li Pengyi alisema ana imani kubwa na maendeleo ya shughuli za uchapishaji nchini China katika siku za mbele. Pia alisema ikilinganishwa na shughuli za uchapishaji za kimataifa, nguvu bora ya shughuli za uchapishaji nchini China inaonekana wazi kutokana na kwamba uchumi wa China unaendelea vizuri, ndiyo maana shughuli za uchapishaji nchini China pia zinaweza kuendelea vizuri; mageuzi ya mfumo wa utamaduni wa China yanasukuma mbele zaidi shughuli za uchapishaji nchini China; aidha sera ya kufungua mlango katika sekta ya utamaduni inazifanya shughuli za uchapishaji nchini China ziwe za kimataifa.
Hisa kubwa ya soko la shughuli za uchapishaji wa China na nguvu zake kubwa za kujiendeleza zinawavutia wachapishaji wengi wa nchi za nje. Mkurugenzi mtendaji wa shirika la uchapishaji la Hachette Livre Bw. Arnaud Nourry alisema, mwezi Aprili mwaka 2009, serikali ya China ilitoa lengo la kuendeleza shughuli za uchapishaji ziwe za kuelekea mahitaji ya soko na zenye nguvu kubwa za kiushindani. Anaona lengo hilo linaonesha kuwa, China siyo tu inakaribisha wachapishaji wa China kuongeza uwekezaji, bali pia inaruhusu wachapishaji wa nchi za nje kuwekeza katika shughuli za uchapishaji nchini China. Alisema lengo hilo linatoa fursa nyingi za kibiashara kwa makampuni ya uchapishaji ya kimataifa, pia inaweka jiwe la msingi kwa ongezeko endelevu la shughuli za uchapishaji nchini China.