Hysteria ni ugonjwa unaotokana na tatizo la afya ya akili. Kihistoria ugonjwa huu ulianza zamani hata kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Jina la ugonjwa huu lilitokana na mawazo ya madaktari wa zamani wa kigiriki waliokuwa wanafikiria kwamba, chanzo cha ugonjwa huu ni matatizo katika mfuko au mji wa mimba wa mwanamke, ambao kwa kigiriki unaitwa ‘hystera’. Hivyo basi madaktari hao waliuita ugonjwa huu kwa jina la ‘Hysterikos’.

Madaktari wa kigiriki walidhani kuwa huu ni ugonjwa unaowapata wanawake pekee. Hii ilitokana na idadi kubwa ya wagonjwa wa tatizo hili kuwa wanawake, na hata pale wanaume walipokuwa na dalili za tatizo la hysteria ilidhaniwa kuwa wana tatizo jingine kwa vile hawakuwa na mfuko au mji wa mimba.

Dhana ya madaktari wa kipindi hicho juu ya ugonjwa huu ilikuwa kwamba mfuko wa kizazi (mji wa mimba) unabana na kukauka kutokana na kutokufanya ngono kwa muda mrefu au kuzidiwa na hamu ya ngono.
Matibabu ya enzi hizo yalihusisha kumtekenya mwanamke katika sehemu zake za siri ili apate kumaliza hamu ya ngono, lakini matibabu hayo yalikuwa hayatowi matokeo ya uponaji yaliyotarajiwa.

Dhana hii ya ugonjwa wa hysteria ingawa ni ya kale sana lakini inaonekana kusadikiwa na watu wengi hata leo. Hata hivyo, sayansi ya tiba ya binadamu imethibitisha kuwa hysteria ni ugonjwa wa akili unaotokana na msongo mkali wa kihisia, ni tatizo la afya ya saikolojia. Tatizo hili hutokea pale mtu anapopata msongo wa kihisia maishani zaidi ya vile alivyojiandaa au anavyoweza kukabiliana nao.

Mara nyingi msongo huu hutokana na hisia au mgogoro wa kifikra, kutokuwa na uhakika wa usalama katika siku za usoni, kutengwa kijamii au kutosikilizwa kwa upendo.Tamaa kali ya kutaka kupendwa kuliko kawaida isipotimizwa, pia huleta tatizo hili pale mgonjwa anapoona kuwa ndani ya moyo wake hakuna akiba yoyote ya kupendwa.

Hysteria huibuka pale sehemu ya akili ndani ya ubongo inapojitahidi bila mafanikio kumlinda muhusika dhidi ya fikra na hisia zinazomsonga. Wakati mwingine hisia na fikra hutokana na matatizo ya kawaida lakini akili huyakuza sana na mhusika akajiona hawezi kuyakabili, hafai na hathaminiwi. Mgonjwa anaweza kujilaumu na kupata hisia za kupoteza ulinzi au kupata kumbukumbu isiyonyamazishwa ya tukio la kinyama alilotendewa.

Watu wanaopata ugonjwa wa hysteria huwa na matatizo ya kihisia ambayo mara nyingi hawapendi kuyazungumzia na kwa sababu hiyo matatizo ya kihisia huwalemea sana. Ingawa watu wa jinsia zote, wakubwa kwa wadogo, hupata tatizo hili lakini wagonjwa wengi ni wanawake hasa wasichana walio kati ya umri wa miaka 12 na18 huathirika zaidi.
Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu mmoja pekee lakini pia unaweza kusambaa kwa wengine katika kundi la watu wanaokabiliwa na msongo wa kisaikolojia unaofanana (mass hysteria or hysterical contagion). Kichocheo cha hali hii huwa ni imani ya kuwa na tatizo au kupata uambukizo kutoka kwa mgonjwa wa kwanza.

Hysteria inayosambaa huanza na mtu mmoja na anapoonyesha dalili, wengine nao huanza kujenga hofu na hisia za kuathirika baada ya kuona mwenzao. Athari hizi katika kundi hutegemea jinsi mtu anavyo tafasri dalili anazoziona na uwezo wake wa kudhibiti msongo. Mara nyingi dalili za hysteria inayosambaa hazionyeshi chanzo bayana na hazitafasiriki sawasawa lakini zinaenea kwa haraka miongoni mwa walioona mgonjwa wa kwanza aliyepata tatizo.
Hofu huongezeka zaidi na tatizo husambaa zaidi pale linapoanza kuhusishwa na imani za kishirikina au mambo ya kimizimu, kupagawa na majini au pepo wabaya. Hofu huzidi pale timu ya wataalamu wa uchunguzi wa vyanzo vya magonjwa wanaposhindwa kubaini chanzo bayana cha tatizo.
Image result for hysteria
Hysteria ingawa ni shida ya afya ya akili lakini pia hudhuru mwili kwa kiwango kikubwa. Hofu, woga na wasiwasi husababisha mapigo ya moyo wa mgonjwa kwenda harakaharaka, kutapika, kupata kichefuchefu, mwili kuishiwa nguvu, maumivu ya kichwa, miguu kufa ganzi, kushindwa kutembea, kupiga makelele au kucheka sana bila sababu za msingi au kupata degedege.
Wagonjwa wengine hupoteza hamu ya chakula, kutopata choo kabisa au kuharisha na wengine hutokwa jasho jingi, kutetemeka, kupumua kwa shida au kushindwa kupumua vizuri kiasi kwamba hewa chafu ya ukaa haitolewi mwilini kwa kiwango cha kutosha. Na hii husababisha kutokea kwa dalili nyingi za mgonjwa mwenye tatizo la hysteria.

Wagonjwa wenye tatizo hili pamoja na mambo mengine wanahitaji zaidi kuonyeshwa upendo wa dhati, kujengewa hisia zitakazowahakikishia usalama, kuaminiwa na kuwaondolea chanzo cha tatizo. Wengi hupata nafuu kutokana na uangalizi wa karibu, upendo wa dhati na dawa za usingizi.