Shukran za dhati kwa SYLIVERY MANYAMA kwa kufanya swali hili
Ni kweli kwamba dhana ya Falsafa hutoshelezwa na matawi yake kwa namna mbalimbali. Wataalamu wametoa maana mbalimbali za Falsafa ambazo kwa namna moja au nyingine zinatosheleza matawi yake. Kiontomolojia neno Falsafa limetokana na maneno mawili ya kigiriki Philo lenye maana Kupenda na Sophia lenye maana Hekima. Hivyo zifuatazo ni fasili mbalimbali kuhusu dhana ya falsafa kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali.
Kwa mujibu wa Sadipo (1973) anafasili Falsafa ni mawazo, fikra na udadisi kuhusu dhana na kanuni zinazotusaidia kuongeza uzoefu kuhusu maadili, dini, maisha ya kisiasa, sheria, saikolojia, historia na sayansi ya jamii. Tunaona kuwa Fasili hii ina mapungufu kwa sababu inachukulia Falsafa kama kanuni zinazotusaidia kuongeza uzoefu lakini sio kanuni zote katika maisha humuongezea mtu uzoefu kuhusu maadili na vitu vingine kwa sababu kuna baadhi ya kanuni humnyima uhuru mwanadamu na kumgandamiza.
Pia Ankipelu (1981) amefafanua maana ya falsafa katika mitazamo miwili ambayo ni Falsafa kama mtazamo na Falsafa kama taaluma. Katika Falsafa kama mtazamo anafafanua kuwa Falsafa ni mtazamo na muono wa mtu binafsi juu ya maisha. Hii hufanya mtu awe na dhana fulani, imani, na fikra fulani juu ya kitu. Anaendelea kusema kila mtu anakitu anachokiona kuwa ni kizuri au kibaya na anachokipenda  au asichokipenda ingawa hali hiyo hutegemea makuzi ya mtu huyu. Fasili hii inataka kutuaminisha kuwa Falsafa ni suala la mtu binafsi tu hivyo ikiwa kuna miono au mitazamo itakayotolewa na kikundi cha watu wenye imani moja basi haitakuwa Falsafa kitu ambacho si sahihi.
Pia Akinpelu anaendelea kufasili dhana ya Falasafa kama taaluma kwa kusema ni mafunzo au nidhamu ya kitaaluma ambayo wanazuoni huwekeza maarifa, muda na nguvu zao. Hufunuliwa na kueleweka kwa kufuata utaratibu fulani wa mawazo yenye maana na mawazo huwepo kujaribu maswali mbalimbali yahusuyo binadamu. Ni kweli kuwa Falsafa huweza kuwa ni mafunzo kwa kuwa pengine hutolewa kwa mafunzo fulani maalumu lakini yeye anajikita katika mafunzo na hajaweka wazi kuwa nini kinatokea baada ya hayo mafunzo ambayo yeye anayaita kuwa ni Falsafa na hayo mafunzo yanakuwa yanahusu nini hasa.
Alexander Nehemas (1985) anafasili Falsafa kuwa ni uwezo na maarifa aliyonayo mtu yanayohusu kujua mambo mengi tofautitofauti. Mambo hayo yanaweza kuwa mazuri au mabaya. Nehemas anazungumzia uzuri na ubaya,yaani ukiwa na uwezo wa kuyafahamu mambo haya basi wewe ni Mwanafalsafa lakini sio kweli kwamba ukiweza kujua mema na mabaya tu basi inatosha kuwa Mwanafalsafa kwa sababu muda mwingine kuna wakati mwanadamu anapaswa kutatua matatizo mbalimbali na sio tu kuyajua kama anavyodai Nehemas.
Thomas Pogge (1989) anaeleza Falsafa ni mtazamo wa ndani wa upendo wa hekima na maarifa. Hekima ni uwezo wa kuuelewa ulimwengu na yaliyomo na yanayotokea, hiyo ndio Falsafa. Yeye anasisitiza kuhusu maarifa lakini kuwepo na upendo. Swali ni je, upendo ni nini? Au tunawezaje kujua kuwa huu ni upendo na huu sio upendo?. Fasili hii inaibua maswali kadhaa ambayo yanaleta mkanganyiko mwingine kwa sababu hakuna ishara yoyote ambayo itatuambia sasa haya ni maarifa ya upendo hivyo iwepo Falsafa na haya sio maarifa yenye upendo kwa hivyo sio Falsafa. Kwa maana hiyo suala la msingi hapa liwe ni uwepo wa maarifa na hekima pekee sio lazima yawe ya namna fulani.
Odera (1990) anasema Falsafa ni taaluma ambayo kanuni za msingi kuhusu asili, binadamu na jamii huchunguzwa na kujadiliwa.Odera anazungumzia taaluma ambayo mtu anapaswa kuwa nayo ili kuchunguza jambo fulani na kanuni zake bila kuzitaja hizo kanuni ni zipi hasa ambazo kimsingi inawezekana kuwa hizo kanuni zenyewe ndizo Falsafa. Kwa maana hiyo, hizo kanuni zinapaswa kuwa ndizo Falsafa yenyewe kwa kuwa ndiyo inayomwongoza binadamu kuishi.
David Papineau (1993) anaeleza Falsafa ni fikra za ndani kabisa kuhusu maswali magumu ambayo yapo. Mara nyingine unaweza ukadhani kama wanasayansi wanaweza kuyajibu kwa ushahidi lakini hata ushahidi huo ukakosa ushahidi wa uwepo wake. Hivyo tunaona kuwa suala la msisitizo katika fasili hii ni fikra za ndani kwa mujibu wa Papineau akimaanisha kuwa hizi ni fikra tu na ikiwa ni fikra tu za ndani basi ni vigumu kujua kama huyu mtu anawaza kuhusu jambo fulani. Kwa maneno mengine ni kuwa, maswali hayawezi kupata majibu kwa kuwa majibu yamebaki kuwa fikra tu za mtu binafsi ambazo watu wengine hawawezi kuziona. Labda hoja ya msingi ibaki kuwa fikra lakini fikra hizo ziwasilishwe na muhusika kwa ajili ya kupata majibu ya maswali mbalimbali.
Simon Blackburn (1994) anafafanua Falsafa kuwa ni mchakato wa kutengeneza mawazo yaliyo katika utaratibu maalumu yanayotoa tafakuri juu ya ulimwengu, kile kinachofanya uwe vile tunavyoona. Hujaribu kutazama sababu, muda, hiyari, anga na mengine mengi. Mwanafalsafa huyu anaeleza kuwa ni mawazo yaliyo katika utaratibu malumu kitu ambacho ni sahihi lakini hajafafanua zaidi kuwa nini kifanyike baada ya kuzifahamu sababu hizo na kuna kweli gani kuhusu sababu hizo. Kwa hiyo ingekuwa vyema zaidi kama mawazo na sababu hizo ambazo zimepatikana kama anavyosema Blackburn zingepimwa kama kuna ukweli wa sababu hizo ndipo mawazo hayo yawe Falsafa ikiwa hicho hasa ndicho alicholenga kukisema.
Paul Snowdon (2014) anafasili dhana ya Falsafa kuwa ni jumla ya majibu yote yanayotolewa juu ya maswali mbalimbali yanayohoji uhalisia wa ulimwengu na maarifa yake kwa kutafuta ushahidi. Snowdon anajikita zaidi katika majibu kitu ambacho ni sahihi kwamba majibu ndiyo yanayofanya watu wafahamu vitu mbalimba. Pamoja na hayo, mwandishi huyu hakutazama upande mwingine wa sarafu kuwa hakuchunguza hata ni nini kimetumika kuleta majibu hayo. Vilevile sio majibu pekee ndiyo yanahitajika katika ulimwengu, muda mwingine hata mafunzo tu yanahitajika juu ya ulimwengu. Hivyo alipaswa kujua kuwa hata majibu hayo yalitumia mawazo na maarifa fulani kupatikana ambayo nayo yanaweza kuwa Falsafa.
Hivyo kutokana na fasili za wataalam mbalimbali kwa mawazo yetu tunaona kuwa Falsafa ni Maarifa, miongozo yenye hekima na mawazo ambayo jamii au mtu huamini kuwa ni kweli na kufanya kuwa moja ya misingi katika maisha yake. Vilevile kupitia maarifa hayo ndipo tunaweza kupata utatuzi wa maswali na changamoto mbalimbali zinazohusu jamii na ulimwengu kwa ujumla. Changamoto hizi zinaweza kuwa ni za kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni.
Baada ya kuangalia fasili za wataalamu mbalimbali kuhusu Falsafa pamoja na mtazamo wetu, yafuatayo ni matawi ya Falsafa na jinsi yanavyotosheleza dhana za Falsafa za wataalamu mbalimbali.
Metafizikia.
Kwa mujibu wa Akinpelu (1981) anasema neno metafizikia linatokana na maneno mawili yani “meta” lenye maana baada na “Fizikia” lenye maana Ulimwengu. Haya yalisemwa na Andronicus ambaye alikuwa anafuata mafundisho ya Aristotle kuhusu mipaka ya ulimwengu. Pia Joseph Omoregbe (1999) anaweka wazi kuwa Metafizikia hutazama nanma ulimwengu ulivyo na matatizo yake na namna ya kuyatatua na ukweli wa mambo kuhusu ulimwengu. Hivyo tunaona kuwa tawi la metafizikia lenyewe likiunga mkono fasili iliyotolewa na Bluckburn (ametajwa) ambapo huchunguza namna ulimwengu ulivyo pamoja na mipaka yake. Anaelezea mambo yanayohusu juu ya kuwapo kwa ulimwengu na kile kinachofanya uwe vile tunavyouona ulimwengu, kwa hiyo tunaona fasili ya bluckburn imetoshelezwa  na tawi la metafizikia.
Mantiki.
Kwa mujibu wa Luke Mastin (2008) anasema hii ni taaluma inayohusu fikra. Taaluma hii huwa na miundo ya fikra juu ya dhana mbalimbali, na huweza kuchunguza kanuni au hoja zilizo sahihi na zisizo sahihi.Hufafanua fikra hizo kwa kufuata utaratibu fulani wa mawazo yenye maana na mawazo hayo huwepo kujaribu kujibu maswali mbalimbali yahusuyo binadamu. Hivyo tunaona tawi hili linatosheleza dhana ya falsafa ya Akinpelu anaesema Falsafa humfanya mtu awe na dhana fulani, imani na fikra fulani juu ya kitu.
Maadili.
Mastin (2008) anasema ni taaluma inayochunguza kuhusu lipi la kufanya na lipi si la kufanya. Tawi hili linachunguza mwenendo wa mtu au jamii kimaadili. Huelekeza ni namna gani watu wanapaswa kuishi, yapi ni maadili mema na yapi ni mabaya. Tawi hili kwa ujumla huchunguza mwenendo wa mtu na jamii kimaadili. Tawi hili linatosheleza fasili iliyotolewa hapo awali na Nehemas (ametajwa) alipoeleza kuwa falsa ni taaluma yenye maarifa ya kumruhusu mtu kujua mambo mengi tofauti tofauti ambapo mambo hayo yanaweza kuwa mazuri au mabaya.
Ujumi.
Kwa mujibu wa Baumgarten (1986) akimnukuu Leibniz anasema ni tawi la falsafa linaloshughulika na dhana ya uzuri, ubaya na ukweli wa kitu fulani au mtu fulani. Hupambanua juu ya hisia fulani katika ufahamu wa wanaadamu na usahihi wake katika kutoa tafsiri hasa ya uzuri wa kitu. Hapa ana maana kuwa, kila mtu anaweza kulichukulia jambo fulani katika mtazamo wake. Wapo watu wanaoweza kulichukulia jambo fulani kimtazamo hasi hali ambayo haiwezi kuuondoa mtazamo wa watu wengine wanaolichukulia jambo hilo katika mtazamo chanya. Tawi hili linatosheleza fasili ya Akinpelu ( ameshatajwa) anasema kwamba falsa ni mtazamo na muono wa mtu juu kitu fulani juu ya uzuri wa kitu fulani. Anaongeza kwa kusema,kila mtu ana kitu anachokipenda na asichokipenda na hutegemea makuzi ya mtu huyo.

Epistemolojia
Kwa mujibu wa Harnad (2005) katika kitabu cha Stanford Encyclopedia of Philosophy  anasema kuwa Epistemolojia ni taaluma inayohusu upatikanaji wa maarifa na kuyachunguza maarifa hayo. Epistemolojia hujaribu kujibu baadhi ya maswali ambayo huhoji chanzo na chimbuko la maarifa na ukweli wa maarifa hayo. Pia huchunguza mfumo mzima wa maarifa na mipaka yake. Kwa mujibu wa maelezo haya tunaona wazi kuwa fasili hii ya Epistemolojia inatosheleza fasili ya Falsafa ya Snowden (ameshatajwa) kwamba Falsafa ni jumla ya majibu yote yanayotolewa juu ya maswali mbalimbali yanayohoji uhalisia wa ulimwengu na maarifa yake kwa kutafuta ushahidi wa mambo hayo.
Kwa ujumla tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa Falsafa inahusika moja kwa moja na maisha ya binadamu na ni wazi kuwa Falsafa haiwezi kutenganishwa na maisha ya binadamu. Historia ya Falsafa inaenda sambamba na historia ya binadamu ulimwenguni hata kabla wasomi na wanazuoni hawajagundua kuwa hiyo ndiyo Falsafa. Hii ni sawa na kusema kuwa ili maisha ya binadamu yakamilike yanahitaji misingi,maarifa na kanuni fulani katika maisha yake ambayo inaweza kutatua changamoto mbalimbali za binadamu ambayo ndiyo Falsafa yenyewe.










MAREJELEO
Akinpelu, J. A. (1981). Introduction to Phylosophy Education. London: Madhullan Publisher  
                                     Ltd.
Baumgarten, A. (1986). Sacrifice in Religious Experience. Leiden: Brill Publisher.
Blackburn, S. (1994). The Oxford Dictionary of Philosophy. British: Oxford University Press.
Harnad & Stevan. (2005). Encyclopedia of Philosophy. China: Macmillan
Mastin, L. (2008). A Cultural Journey through the English Lexicon. IGI Global
Nehemas, A. (1985). Life as Literature. Havard University Pre
Odera, H. (1990). Trends in Contemporary African Philosophy. Nairobi: Shirikon Publishers
Omeregbe, J. L. (1999). Metaphysics Without Tears. Lagos: Research Publication.
Papineau, D. (2009). Philosophy. Duean Barid Publisher
Paul, F. (2014). Persons, Animals, Ourselves. Oxford University Press.
Pogge, T. (1989). Realizing Rawls. New York. Cornell University Press.
Sadipo. (1973). Woman and African Society. France: Strabourg.