MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewapandisha kizimbani Boniface Jacob na Godlisten Malisa wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuchapisha na kusambaza taarifa za uongo mtandaoni kinyume cha sheria.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Mei 6, mwaka huu nakusomewa mashtaka yao na wakili wa serikali Happy Mwakamale akishirikiana  na Neema Moshi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Ushindi Swallo.
Akisoma hati ya Mashtaka Wakili Mwakamale amesemaa wameshatakiwa chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015 inadaiwa kuwa, mnamo Aprili 22 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa makusudi ya kupotosha umma Jacob alichapisha ujumbe wenye taarifa za uongo kupitia mfumo wa kompyuta uitwao X wenye jina la Boniface Jacob@ExMayorUbungo.
Amefafanua kuwa mnamo Machi 19 mwaka huu kwa kujua na kwa nia ya kupotosha umma Jacob pia alichapisha taarifa za uongo kupitia mfumo wa kompyuta uitwao X wenye jina la Boniface Jacob@ExMayorUbungo.
Katika shtaka la tatu linalomhusu mshtakiwa wa pili, mnamo Aprili 22 mwaka huu  kwa kujua na kwa lengo la kupotosha umma alichapisha ujumbe wenye taarifa za uongo kupitia mtandao wa Instagram wenye jina la Malisa-gj.
Hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 6 mwaka huu itakapoitwa kusikilizwa, washtakiwa  wote wawili wapo nje kwa dhamana.