SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limesema kuwa linaanza kutoa rasmi gazeti maalum ambalo litazungumzia masuala mbalimbali ya wafanyakazi nchini ambalo lifahamika kwa jina la ‘Mfanyakazi Tanzania’.

TUCTA imesema gazeti hilo linatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya Sherehe za Mei Mosi Kitaifa 2024 yatakayofanyika jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya amesema kuwa gazeti hilo linamilikiwa na shirikisho hilo na kusimamiwa na Kampuni Tanzu inayoitwa Workers Development Corporation (WDC).

Amesema kuwa kipindi cha nyuma TUCTA ilikuwa na chombo chake cha habari ambacho ni gazeti lililokuwa maarufu sana na lilikuwa linaitwa gazeti la Mafanyakazi.

“Hiki ndicho chombo cha habari kilichokuwa kinatumika na Vyama vya Wafanyakazi katika kutoa habari kwa wafanyakazi na umma kwa ujumla kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii, uchumi, siasa, kimataifa, burudani na michezo.

“Gazeti hili lilikuwa likitoka mara mbili kwa juma kwa siku za Jumatano na Jumamosi, lakini baadae, kutokana na changamoto za kiundeshaji, likawa linatoka mara moja kwa wiki. Lakini kuanzia mwaka 2012 gazeti hilo likashindwa kuendelea kutokana na sababu mbalimbali,” amesema Nyamhokya

Amesema TUCTA kupitia vikao vyake vya kikatiba imetafakari upya umuhimu wa kufufua gazeti lake la mfanyakazi na hivyo mchakato ulifanyika na wamefanikiwa kupata usajili kutoka Idara ya Habari – Maelezo Machi 27, 2024 ambapo kwa sasa gazeti hilo litajulikana kwa jina la “Mfanyakazi Tanzania”.

Hata hivyo amesisitiza kuwa gazeti la Mfanyakazi Tanzania ni la kisasa linalolenga kutoa habari na kuelimisha kundi la wafanyakazi na watanzania kwa ujumla kuhusu masuala mbalimbali.

“Mpango uliopo ni kwamba gazeti hili litakuwa linasambazwa kwa machapisho na mitandaoni,” amesema