Henock Inonga.

HABARI mbaya kwa mashabiki wa Simba ni kwamba beki wao wa kati Henock Inonga Baka yupo katika hatua za mwisho za kumalizana na Klabu ya FAR Rabat ya nchini Morocco ambayo inanolewa na Kocha Nassredine Nabi.

Nabi anamfahamu vyema beki huyo kwa kuwa amemshuhudia zaidi katika kikosi cha Simba kipindi ambacho yeye alikuwa kocha wa Yanga.

Chanzo cha ndani kutoka DR Congo kimeeleza juu ya Inonga Baka akiwa katika kambi ya AFCON tayari amekuwa na mazungumzo na mabosi wa FAR Rabat ambao wamemfuata tayari kwa ajili ya mazungumzo naye kisha uongozi wa Simba.

“Inonga bado anamkataba wa kuitumikia Simba na tayari mchakato wa yeye kutaka kuondoka ndani ya timu hiyo umeanza kwa viongozi wa mchezaji na uongozi wa timu ya FAR Rabat kuwa katika mazungumzo yao lakini pia utakuwa kuwahusu viongozi wa Simba.

“Simba wao wanamhitaji bado Inonga Baka lakini kama litakuja dau au itakuja ofa nzuri basi naamini kuwa kila kitu kitakwenda sawa kwa maana ya kumuuza kama ambavyo iliwahi kuwauza kina Luis Miquissone na Clatous Chama,” kilisema chanzo hicho.

Kwa upande wa Ahmedy Ally Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba alisema kuwa: “Sisi kama Simba taarifa zetu huwa tunazitoa sehemu sahihi hayo mambo ya tetesi kwetu hatuwezi kuyazungumzia kwa kuwa hatuwezi kuzungumzia tetesi badala ya uhalisia wa jambo lenyewe.”