Habari za Michezo leo

Kikosi cha JKT Tanzania kimeanza rasmi mazoezi na kambi kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kurejea kupigwa tena katikati ya mwezi ujao, huku kiungo Hassan Dilunga, akimkaribisha mchezaji mwenzake wa zamani wa Simba SC, Shiza Kichuya.

Kichuya ni mmoja wa wachezaji waliojiunga na kikosi cha JKT Tanzania kipindi cha dirisha dogo kilichomalizika Januari 15, akitokea Namungo FC.

Kikosi hicho kilianza mazoezi yake rasmi juzi Jumamosi (Januari 20) kwenye Ufukwe wa Coco, Dar es salaam baada ya mapumziko ya siku kadhaa.

“Shiza Ramadhani Kichuya, kona goli, karibu sana JKT Tanzania, karibu kwenye familia yetu, nakutakia kila la heri nakufahamu mwanangu, tena uko na wanao hapa, nipo mimi Ndemla (Said), hautakuwa mgeni, nadhani utauwasha kama kawaida yako,” Dilunga amemkaribisha Kichuya ambaye alimjibu kwa kushukuru.

Dilunga ambaye kwa sasa ameanza mazoezi mepesi baada ya kuumia katika moja ya mechi ya Ligi Kuu, alijiunga na timu hiyo akitokea Simba SC.

Wachezaji hao wote wawili waliichezea Simba SC  na kuipa mafanikio makubwa timu hiyo.

Akizungumza baada ya kukaribishwa kwenye kikosi hicho, Kichuya amesema atapambana ili kuhakikisha JKT Tanzania inatimiza malengo.

“Kikubwa naamini uwezo wangu, popote nitakapokuwa nacheza ndiyo kazini kwangu, nilikuwa Mtibwa nimetoka, Simba nimeondoka, Namungo pia sasa ni mchezaji wa JKT Tanzania nimekuja kuongeza nguvu na wanajeshi wenzangu ili kuipeleka timu ambapo mashabiki wa JKT Tanzania wanahitaji ifike, nina imani tufanya vema kutokana na usajili ambao viongozi wameufanya hasa huu wa maingizo mapya,” amesema winga huyo.