NGUVU ZA HOJA: Lugha ya Kiswahili ina uwezo wa kuimarisha umajumui wa mataifa ya bara zima la Afrika

NGUVU ZA HOJA: 

NA PROF CLARA MOMANYI

KARNE chache zilizopita, Kiswahili kilichukuliwa kama lugha ya watu wa chini kijamii.

Kilichukuliwa kama lugha isiyoweza kumhakikishia mtu maisha bora au hata elimu ya kumwinua kiuchumi.

Kuna waliodhani kwamba hii ni lugha isiyoweza kudhibiti mafunzo ya sayansi ati kwa sababu haikuwa na msamiati au hata istilahi za kuweza kufanikisha maendeleo yoyote kwa wenyeji wake.

Kutokana na hatua zilizopigwa katika kuimarisha na kueneza lugha hii kama chombo cha maendeleo na uchumi, hoja hizo za awali sasa zimekuwa muflisi katika ulimwengu unaokumbatia uanuwai wa lugha na maendeleo kwa ujumla.

Katika Afrika Mashariki ambako ndiko kwenye chemchemi za Kiswahili, kuna shinikizo ambazo zinaendelea kutolewa ili kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi si tu katika eneo hili, bali pia kama lugha ya kuimarisha umajumui wa bara la Afrika.

Nchini Afrika Kusini, kwa mfano, kiongozi wa upinzani Bw Julius Malema ni mmoja wa wale wanaoshabikia ukuaji wa Kiswahili barani Afrika.

Hivi majuzi alipokuwa akitoa hotuba kuhusu umuhimu wa kufundisha na kujifunza Kiswahili kama lugha ya kimataifa, aliwataka Waafrika barani kukienzi Kiswahili kama lingua franka ya Afrika.

Katika nchi jirani ya Tanzania, licha ya tetesi zisizothibitika kwamba Kiingereza sasa kinapewa umuhimu zaidi kuliko Kiswahili, serikali ya Tanzania ilijitoa kimasomaso na kutangaza kwamba kuna mipango ya ujenzi wa chuo kikuu cha Kiswahili katika eneo la Bagamoyo. Nako nchini Uganda, kuna hoja iliyokubaliwa bungeni kwamba Kiswahili kitumike kama lugha rasmi nchini humo.

Hii ni kufuatia uamuzi uliotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwamba Kiswahili, Kifaransa na Kiingereza ziwe lugha rasmi za shughuli katika Jumuiya hiyo.

Chanzo: Taifaleo