• Wametakiwa kuwasiliana na vyuo vyao na kufuatilia taratibu za kupata visa kabla ya kupanga safari ya kurudi nyumbani Tanzania.
  • Mwanafunzi atakayerudi Tanzania kipindi hiki hataweza kurudi China hadi hapo nchi hiyo  itakapoanza tena kutoa vibali vya makazi kwa raia wa kigeni. 

Dar es Salaam. Ubalozi wa Tanzania nchini China umewataka wanafunzi wanaosoma katika jiji la Wuhan nchini humo kuwasiliana na vyuo vyao na kufuatilia taratibu za kupata visa kabla ya kupanga safari ya kurudi nyumbani Tanzania.
Hatua hiyo inafuatia kuondolewa kwa marafuku ya kusafiri katika jiji hilo liliko katika jimbo la Hubei leo (Aprili 8, 2020) ambalo ndiyo kitovu cha mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona unaosambaa kwa kasi duniani.
Taarifa ya ubalozi huo iliyotolewa leo, imeeleza kuwa wanafunzi wanaosoma katika jiji hilo wenye nia ya kurudi Tanzania wanapaswa kuwasiliana na vyuo vyao ili kufahamu taratibu za kuruhusiwa kusafiri nje ya nchi na tarehe ya kufungua vyuo.
Imeeleza kuwa wanatakiwa kuzingatia uamuzi wa China wa kufuta kwa muda visa na vibali vya makazi kwa raia wa kigeni ikiwa ni hatua ya kukabiliana na virusi vya COVID-19 kutoka nje.
“Hivyo, mwanafunzi atakayekwenda Tanzania kipindi hiki hataweza kurudi China hadi hapo Serikali ya China itakapoondoa zuio lake,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa leo jijini Beijing, China.
Aidha, wanafunzi hao wanaweza kutumia usafiri wa Shirika la ndege la Ethiopia ambalo hufanya safari mara moja kwa wiki siku ya Jumatatu kwa sababu huo ndiyo usafiri pekee wanaoweza kuutumia kurudi Tanzania.
Na hata wakirudi nyumbani, watatakiwa kukaa karantini kwa siku 14 katika eneo maalum kama mwongozo wa Wizara ya Afya unavyoelezwa kwa wasafiri wote wanaoingia nchini kuanzia Machi 25, 2020. 

Endapo baada ya kuondolewa marufuku ya kusafiri, wanafunzi wakikabiliwa na changamoto zozote, jumuiya zao zinapaswa kuwasiliana na ubalozi huo ili kutafuta ufumbuzi.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) tangu kuanza kwa ugonjwa huo mwishoni mwa mwaka 2019 hadi jana (Aprili 7, 2020) China imeripoti visa 83, 071 vya wagonjwa wa Corona ambapo watu 3,340 wamefariki dunia kwa ugonjwa huo. 
Hata hivyo, wakati wakiwa nchini humo wametakiwa kuendelea kufuatilia na kutekeleza tahadhari zinazotolewa na China ikiwemo kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka kugusa pua, macho au mdomo na kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya. 
Februari 12, 2020, Serikali ya Tanzania ilitangaza kutowarejesha nchini wanafunzi 420 waliopo mji wa Wuhan nchini China kwa kuwa nchi zilizofanya hivyo zilisababisha kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona katika nchi husika.