KAMA Emmanuel Okwi anayelipwa Mil. 15 kwa mwezi au Meddie Kagere atakayedaka Mil. 12 anataka kuvunja mkataba na Simba ya mwekezaji msomi, Mohammed Dewji ‘MO’ lazima kijasho kimtoke.
MO ambaye ni bilionea, kwenye mikataba yote ya wachezaji wa Simba ameweka kipengele kwamba kama mchezaji anataka kuvunja mkataba atalipa dola 600,000 ambazo kwa hela ya madafu ni Sh.Bilioni 1.5.
Gharama hiyo ni sawa na thamani ya kikosi cha Simba kilichotwaa ubingwa msimu uliopita kwa kupoteza mchezo mmoja tu mbele ya Rais John Pombe Magufuli kwenye Uwanja wa Taifa.
Habari za ndani zinasema kwamba Simba wamekubaliana kuweka kipengele hicho ili kuondokana na janga la kupoteza wachezaji wazuri na kuhakikisha kuwa kikosi hicho kinakuwa imara.

“Mchezaji akivunja mkataba kwa sasa lazima alipe dola 600,000 kimewekwa hicho kipengele ili kuwadhibiti, inafikaga wakati klabu inapoteza wachezaji wazuri kirahisi sana,”alisema mmoja wa vigogo wa Simba. Aliongeza kwamba lengo la kipengele hicho siyo kukomoa wachezaji bali kuhakikisha klabu inanufaika na hata kuzuia wapinzani wake kuibomoa kirahisi.
Habari zinasema kwamba MO ameitengeneza mikataba hiyo kisomi ili kuhakikisha kwamba Simba inadumu na wachezaji wake muda mrefu ili kujenga kikosi imara kama zilivyo timu kubwa za Afrika. Habari za uhakika zinasema kuwa hata masilahi na posho za wachezaji zitaboreshwa ili wasiingiwe na tamaa ya kuondoka Msimbazi. Kama mchongo huo utatekelezeka Simba itakuwa ndiyo klabu ambayo itahamisha wachezaji wake kwa bei ghali zaidi nchini kwani klabu zingine hazina kipengele hicho.