na EMANUEL MASSHELE Machi 2016 DHANA YA UELEKEZI (TRANSITIVITY) Dhana ya uelekezi imefafanuliwa na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo: Vitenzi elekezi ni vitenzi ambavyo havijitoshelezi kisarufi vinahijia kutoshelezwa na yambwa moja au mbili ili vijikamilishe kisarufi (W.H.Whitely). Nomino inayokuja baada ya kitenzi inashikamana vipi na kitenzi husika. Ufafanuzi mpana wa dhana ya uelekezi unajikita katika namna mbalimbali za kukamilisha vitenzi. Massamba (2004) anafafanua uelekezi kuwa ni uhusiano uliopo baina ya kitenzi na vijenzi vingine vya kimuundo wa sentensi vinavyohusiana nacho. Habwe na Karanja (2004) wanaeleza kuwa uelekezi ni hali ya kitenzi kuruka mipaka na kuathiri maneno mengine ya sentensi. Maneno hayo yanayoathiriwa huwa ni yambwa au yambiwa. Kihore (2001) anaona uelekezi kuwa ni uwezo wa kitenzi kinachoundwa na mzizi fulani kuchukuana na yambwa katika muundo wa sentensi. Wren na Martin (2007) wanafasili kuwa uelekezi ni hali ya kitenzi kuashiria tendo linalofanywa na mtenda au kiima likiwa na yambwa. Mkude (1995) anafafanua uelekezi kuwa ni uwezo wa kitenzi kujitosheleza kimuundo yaani iwapo kitenzi kinahitaji kujalizwa na kipashio kingine ili kifanye kazi kikamilifu. Kwa ujumla, uelekezi ni dhana inayohusu hali ya kitenzi kubeba au kutobeba yambwa au yambiwa. Ni dhahiri kuwa dhana ya uelekezi ina uhusiano wa moja kwa moja na na kikundi tenzi. Hivyo ni vyema kukielewa vizuri kitenzi cha Kiswahili. Kitenzi ni kategoria ambayo ni muhimili wa kikundi tenzi cha Kiswahili, ni nguzo au kielelezo muhimu cha sifa bainifu za lugha ya Kiswahili. Pamoja na kudokeza uelekezi, kitenzi cha Kiswahili hudokeza pia mambo mbalimbali kama vile kauli,njeo, hali nk. AINA ZA VITENZI Kwa kutumia kigezo cha uelekezi, wanasarufi wanagawa vitenzi vya Kiswahili katika makundi mawili nayo ni: Vitenzi si elekezi Vitenzi elekezi. i.Vitenzi si elekezi Hivi ni aina ya vitenzi ambavyo havihitaji kujalizwa na yambwa au yambiwa (kiathirika na mnufaikaji/ mfaidikaji) ili kukamilisha maana katika sentensi kama inavyooneshwa katika mifano ifuatayo: Juma mto umejaa Mbuzi amekufa Ndege ameruka Juma ameoa Giza limeingia Cesilia analia Riziki anakoroma Kikombe kimevunjika Mvua zinanyesha Easter amenuna nk. Vitenzi katika sentensi hapo juu (a) hadi (f) hazihitaji yambwa kwa kuwa vitenzi vyenyewe vilivyotumika vinajitosheleza kimawasiliano (kimaana). Hatuwezi kwa mfano katika sentensi hizo tukabaki tunajiuliza maswali ambayo ni lazima yajibiwe. Mifano zaidi ya vitenzi hivyo ni duwaa, kua, zaa, ngaa, imba, kaa nk. Vitenzi elekezi Hivi ni vitenzi ambavyo huhitaji kujalizwa na nomino moja au mbili. Kwa maneno mengine, vitenzi elekezi ni vile vyenye uwezo wa kungoeka/ kubeba yambwa na/ au yambiwa. Vitenzi elekezi vyaweza kuwa elekezi kwa hulka yake au kwa kunyambuliwa. Unyambulishaji unaweza kuathiri kitenzi sielekezi kuwa elekezi kwa kukiongezea, kupunguza au kudhibiti vihusika vinavyoambatana nacho. Vitenzi elekezi vimegawanyika katika makundi mawili nayo ni: Vitenzi elekezi mara moja Vitenzi elekezi mara dufu Vitenzi elekezi mara moja. Hivi ni vitenzi elekezi vyenye kubeba yambwa moja tu. Chunguza mifano ifuatayo: Shoo amejenga nyumba Shembilu amenunua gari Neema ameleta machungwa Dada anapika ugali Vitenzi vilivyomo katika sentesi hizo hapo juu zinahitajia yambwa moja ili kujikamilisha kimawasiliano. Mifano ya vitenzi vyenye hulka sawa na hivyo ni pamoja na beba, penda, iba, shusha, andika, chuma, soma nk. Vitenzi vyote hivyo vina tabia zinazofanana. Vitenzi elekezi mara dufu Hivi ni vile vitenzi ambavyo vinahitaji kujalizwa kwa yambwa mbili ili viweze kujikamilisha kisarufi. Mifano ifuatayo inadhihirisha ukweli huu: Mwenyekiti amempa katibu ujumbe wake Meneja alimkabidhi mhudumu mali zake Jane alimpiga mpenzi wake kofi Mwalimu alimpa mwanafunzi mimba Vitenzi vyote katika sentensi hizo vinahitajia kufuatwa na yambwa zaidi ya moja. Vitenzi elekezi mara dufu siyo vingi sana katika lugha ya Kiswahili ukilinganisha na vitenzi elekezi mara moja. DARAJIA ZA UELEKEZI Uelekezi uko katika darajia mbili ambazo ni utendwa yaani kiathirika na utendewa yaani mfaidikaji/ mnufaikaji. Chunguza mifano ifuatayo: Dada alimchumia baba yake maua Mtoto alimuandikia baba barua Mwajuma anampikia mmewe ugali Nomino zilizokolezwa ni yambwa tendewa ambazo zinanufaika na tendo lenyewe na zile zisizokolezwa ni yambwa tendwa yaani zinzathirika na tendo moja kwa moja. Ikiwa sentensi ina yambwa tendwa na tendewa, basi kitenzi chake hubeba kiambishi cha yambwa tendewa. Iwapo sentensi ina yambwa tendwa tu, basi kitenzi chake pia chaweza kubeba kiambishi yambwa. Kanuni hii inazua utata kuwa ni katika mazingira gani kiambishi yambwa chaweza kuwepo katika kitenzi na kutokuwepo katika kitenzi?? Chunguza mifano ifuatayo: Kova anaikata nyama Edo anamkatia nyama mama Ali anamjengea baba nyumba Fatuma alimnunulia shangazi gari Mama anampikia mgeni ugali Ukilinganisha mifano yote ya vitenzi vyenye uwezo wa kubeba yambwa utaona kuwa tofauti ya kungoeka au kutongoeka yambwa moja au mbili inathiri pia uwezo wa kitenzi kubeba au kutobeba kiambishi yambwa. Ibrahim Kagita at 01:41:00 Shiriki  Hakuna maoni: Chapisha Maoni ‹ › Nyumbani Ona toleo la wavuti Kunihusu  Ibrahim Kagita  With the massive scientific discoveries have made the rational thinking ability of human being to be bound. As a social educator we ought revive the ancient thoughts through education which is based on reasoning, discussion of contraverse ideas,speculation etc. "...if you have a plan of one year plant crops/flowers, if you have a plan of ten years plant trees and if you have a plan of ahundred years educate children." By Conficious Tazama wasifu wangu kamili Inaendeshwa na Blogger.